Sheria za Marekani: Haki za Marekebisho ya Kwanza
Katiba na Muswada wa Haki wa Marekani
Shirikisho la Majimbo ya Marekani lilianzishwa mwaka 1776 wakati wa vita vya mapinduzi dhidi ya Uingereza, nchi ambayo ilikuwa imeitawala Marekani kama makoloni tangu miaka ya 1600. Baada ya uhuru, makoloni yalifanyika kuwa majimbo na wawakilishi kutoka kila jimbo walitunga Katiba ya Marekani ambayo ilianzisha sheria za taifa jipya. Ili kutekelezwa, Katiba ilihitajika kukubaliwa na kila jimbo kupitia uidhinishaji. Uthibishaji wa Katiba mpya ulikumbwa na mjadala mkali, na ingawa hatimaye ulifanikiwa, kila serikali ilikuwa na orodha ndefu ya mabadiliko waliyotaka kufanya katika Katiba. Idadi kubwa ya mabadiliko haya yalihusiana na kulinda haki za watu dhidi ya udhalimu wowote unaoweza kutekelezwa na serikali. Kati ya mabadiliko mengi yaliyopendekezwa, kumi yaliongezwa katika Katiba kama Marekebisho mwaka 1791. Marekebisho haya kwa kumi ya kwanza yanajulikana kama Muswada wa Haki. Marekebisho zaidi yaliongezwa baadaye na, ingawa ni vigumu, Katiba inaweza kubadilishwa tena katika siku zijazo.
Marekebisho wa Kwanza
Marekebisho ya kwanza yanasema kwamba serikali haiwezi kumnyima mtu uhuru wa kuabudu kulingana na dini yake yoyote iwayo. Pia inaikataza serikali kuzuia uhuru wa kuzungumza, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kukutana na kuishinikiza serikali. Aidha, Marekebisho ya Kwanza yanaikataza serikali “kuanzisha dini”, ambayo inamaanisha serikali haiwezi kukuza, kuidhinisha au kugandamiza dini yoyote.
Aina Tano za Uhuru
Uhuru wa Dini
unawaruhusu watu binafsi kuabudu kulingana na imani zao za kidini bila kuingiliwa na serikali. Uhuru huu pia hulinda haki ya mtu ya kuabudu kulingana na dini yoyote, ikiwa ni pamoja na kuwa mtu asiyeamini Mungu.
Uhuru wa Usemi
unalinda haki ya mtu binafsi ya kutoa maoni yake hadharani hata kama ni kuikashifu serikali. Pia unajumuisha usemi wa kitaswira kama vile kuvaa T-shati iliyo na kauli mbiu au kuweka bango mbele ya nyumba yako
Uhuru wa Waandishi wa Habari
unawalinda waandishi wa habari na mashirika ya habari dhidi ya udhibiti wa serikali.
Uhuru wa Kuandaa Mikutano ya Amani
unawaruhusu watu kukusanyika katika maeneo ya umma na kutoa maoni yao kwa pamoja mradi tu wanafanya hivyo kwa amani.
Uhuru wa Kuishinikiza Serikali
unawaruhusu watu binafsi au vikundi kutoa ombi rasmi kwamba serikali ya mitaa, jimbo au kitaifa kushughulikia malalamiko au udhalimu ulioelezwa kwa kufanya mabadiliko ya sheria au kanuni zilizopo.
Vizuizi vya Marekebisho ya Kwanza na Sheria za Serikali
Kuna hali chache muhimu ambazo zinasababisha kunyima uhuru uliolindwa chini ya Marekebisho ya Kwanza. Ni kinyume cha sheria kutoa vitisho, kuhamasisha watu wazue vurugu za haraka, au kupendekeza mapinduzi ya kivita ya serikali. Serikali inaweza kuwahitaji watu wapewe kibali cha kuandaa mikutano na kuweka vikwazo vya wakati na mahali pa kuandaa mikusanyiko mikubwa ili kudhibiti trafiki na kuzuia machafuko ya umma. Pia kuna vikwazo vingine vinavyohusiana na uovu na ponografia. Uhuru wa dini haulindi vitendo ambavyo vimepigwa marufuku na sheria zinazowalinda watu, kama vile ukeketaji wa wanawake, ambao ni tendo la kinyume cha sheria nchini Marekani.
Ufafanuzi wa haki za Marekebisho ya Kwanza wakati mwingine husababisha mabishano ambayo yanapaswa kutatuliwa mahakamani. Sheria kuhusu uhuru wa dini na kutoa maoni hutofautiana kutoka jimbo moja hadi lingine, lakini yote yanatakiwa kufuata Marekebisho ya Kwanza. Mahakama Kuu ya Marekani inaweza kuamua kama sheria ya serikali inakiuka Marekebisho ya Kwanza, na kama ni hivyo, jimbo linahitajika kubadilisha sheria hiyo kinzani. Ni muhimu kujua na kuelewa sheria za jimbo unamoishi ili ujue jinsi zinaweza kukulinda na uweze kuzitii.